DRC :Mtu mmoja apatikana na virusi vya Ebola Goma

0
140

Serikali ya DRC imetoa tahadhari kwa raia wa Goma na vunga vyake kuwa mtu mwenye virusi vya Ebola amepatikana baada ya kufanyiwa ukaguzi katika kituo kimoja mjini Goma muda mfupi baada ya kuwasili kutoka Butembo jana Jumapili.

Kwa mujibu wa wizara ya afya ya DRC, mtu huyo ambaye ni Mchungaji alisafiri umbali wa kilomita zaidi ya 200 kutoka Butembo hadi Goma kwa basi, na inasadikiwa kuwa alikuwa amekutana na watu wenye ugonjwa Ebola.

Hata hivyo wizara ya Afya inasema kwamba hatari ya kusambaa kwa Ebola katika sehemu nyingine za mji wa Goma ni ndogo.

“Dereva wa basi na abiria wengine 18 wanatarajiwa kutpewa chanjo leo Jumatatu”, wizara ya afya imeongeza katika taarifa yake.

Wakaazi zaidi ya milioni moja wanaoishi katika mji wa Goma wameanza kuingiliwa na hofu kwa mujibu wa chanzo kimoja kutoka moja ya mashirika ya kiraia mjini humo.

Ebola huwaathiri binaadamu kupitia mgusano na wanyama walioathirika kama tumbili, na popo wa msituni.

Watu huambukizwa kwa njia ya kugusana, njia ya mdomo na pua, pia kwa njia ya damu, matapishi, kinyesi, majimaji ya kwenye mwili wa mtu mwenye Ebola.

Ebola ni ugonjwa unaoambukizwa na virusi ambapo aliyepata maambukizi hupata dalili za homa, uchovu, maumivu ya viungo na koo.

Pamoja na RFI

ACHA JIBU

Please enter your comment!
Please enter your name here